1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Viongozi wa Ulaya wakutana na Xi Jinping

11 Desemba 2023

Rais wa China Xi Jinping amekutana na viongozi wa Ulaya mjini Beijing, kwa ajili ya mazungumzo ya kina yatakayohusu kila kitu kuanzia biashara hadi vita vya Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Zshk
Viongozi wa China na Umoja wa Ulaya  wakiwa katika mazungumzo mapana Alhamisi ambayo yamejumuisha mizozo yao kuhusu biashara na mgawanyiko mkubwa kufuatia vita nchini Ukraine. Katika picha hii iliyochapishwa na Shirika la Habari la Xinhua, Rais wa China Xi Jinping, wa pili kulia, akizungumza na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, wa tatu kushoto, na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, wa nne kushoto, wakati wa mkutano wao kwenye ukumbi wa mikutano Jimbo la Diaoyutai mjini Beijing, Alhamisi, Disemba. 7, 2023.
Mkutano wa rais wa China na viongozi wa Umoja wa Ulaya uliofanyika Beijing Disemba 7, 2023Picha: Liu Bin/Xinhua/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano wao uliofanyika mapema leo, Rais Xi amesisitiza umuhimu wa uhusiano wa nchi yake na Umoja wa Ulaya, na kusema pande hizo mbili zinapaswa kuwa washirika wanaonufaishana, kuendeleza uaminifu wakisiasa na kujenga muafaka wa kimkakati. 

Rais Xi jinping amesema wanapaswa kuzingatia msimamo sahihi wa ushirikiano wa kimkakati. ''China na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuwa washirika katika ushirikiano wa kunufaishana, kuimarisha uaminifu wa kisiasa daima, kujenga maelewano ya kimkakati, kuunganisha maslahi, kuondokana na uingiliaji wa kila aina, kuimarisha mazungumzo na ushirikiano ili kunufaisha watu wa pande zote mbili. Lazima tushughulikie kwa pamoja changamoto za kimataifa''.

Soma zaidi: Putin akutana na mwenyeji wake Xi Jinping katika mkutano wa mradi wa BRI mjini Beijing

Rais Xi amekutana na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja huo Josep Borrel leo Alhamisi.

Kwa upande wake Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema China ni mshirika muhimu zaidi wa kibiashara wa umoja huo, lakini kuna ukosefu mkubwa wa usawa na tofauti za wazi ambazo lazima zitatuliwe.

Matamshi yake yamekuja baada ya Umoja wa Ulaya  kuitaka China kuboresha upatikanaji wa soko la bidhaa kutoka nchi wanachama wake 27 ili kushughulikia nakisi ya kila mwaka ya biashara ya zaidi ya dola bilioni 200 kati ya pande hizo mbili.

Rais wa China Xi Jinping akipunga mkono anapowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa San Francisco kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa APEC (Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki) huko San Francisco, California, Marekani, Novemba 14, 2023
Rais wa China Xi JinpingPicha: BRITTANY HOSEA-SMALL/REUTERS

China iliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 458.5 kwa Umoja wa Ulaya katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka huu, na kuagiza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 257.8, kulingana na data za mamlaza ya forodha ya China zlizotolewa leo Alhamisi.

Umoja wa Ulaya pia umeikasirisha China kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu ruzuku za zale kwa makampuni ya magari ya umeme ili kubaini kama ruzuku hizo zinawapa wazalishaji nchini China faida isiyo ya haki ya ushindani katika masoko ya Ulaya.

Viongozi hao pia walijadili mada nyingine zikiwemo mabadiliko ya tabianchi na vita vinavyoendelea nchini Ukraine, pamoja na mzozo kati ya Israel na Hamas. Huu ulikuwa mkutano wa kwanza wa kilele wa Umoja wa Ulaya naChina tangu 2019.

Chanzo: AFP