1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Terzic: Tulifanikiwa kuwadhibiti Leverkusen kimbinu

4 Desemba 2023

Kwa mara ya pili msimu huu Bayer Leverkusen wamepoteza pointi katika ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga.

https://p.dw.com/p/4ZlWs
Kandanda Bundesliga | Edin Terzic | Kocha Borussia Dortmund
Kocha wa Borussia Dortmund Edin TerzicPicha: Christof Koepsel/Getty Images

Mara ya kwanza ilikuwa uwanjani Allianz Arena walipotoka sare ya mabao mawili na Bayern Munich kisha hapo Jumapili wakalazimishwa sare ya bao moja na Borussia Dortmund katika uwanja wa Bay Arena.

Leverkusen waliingia katika mechi wakiwa katika msururu wa kushinda mechi 14 na Dortmund ndio waliotangulia kufunga ila kocha wa Leverkusen Xabi Alonso alipompa nafasi Patrick Schick kuingia kama mchezaji wa akiba ndipo mambo yalipobadilika, kwani alisaidia kuunda goli la kusawazisha lililotiwa kimyani na Victor Boniface.

Baada ya mechi hiyo Alonso alikuwa na haya ya kusema.

"Ni vizuri kwamba Patrick yuko nasi na kwa kweli tunastahili kuwa naye akiwa anacheza vizuri. Alicheza dakika 30 wiki iliyopita akafunga bao moja leo amesaidia kuunda bao, kwa hiyo tutamuhitaji Patrick wakati mwengine ashirikiane na Boniface pia ili tucheze na washambuliaji wawili. Lakini kwa ujumla nafikiri timu imecheza vizuri, tumeshinda mechi nyingi na leo tumepata sare. Tulitaka zaidi ila hivi ndivyo ilivyo," alisema Alonso.

Leverkusen kulazimishwa kufanya wasivyopenda

Umuhimu wa Schick kwenye kikosi cha Leverkusen bila shaka umeonekana katika mechi zao mbili zilizopita ila hapo Jumapili Dortmund walihimili shinikizo la goli hilo la wenyeji wao kusawazisha katika kipindi cha pili na kupata sare.

1.Bundesliga, Bayer 04 Leverkusen - Borussia Dortmund  Boniface
Mshambuliaji wa Leverkusen Victor Boniface akifunga goli dhidi ya DortmundPicha: Jan Huebner/IMAGO

Huyu hapa kocha wao Edin Terzic.

"Timu yetu imejituma sana, tumejilinda vyema na kuwalazimisha kufanya vitu wasivyovipenda. Kucheza mipira ya pembe hadi pembe, kuwacha nafasi katikati na kutumia wingi. Halafu wakashindwa kufunga katika lango letu kwa kipindi kirefu cha mechi. Tuliingia uongozini ila hatuakueza kufunga bao la pili. Kumekuwa na maamuzi muhimu dhidi yetu leo na hilo ni jambo ambalo si haki," alisema Terzic.

Bayer Leverkusen kwa sasa wana pointi 35 kutokana na mechi 13, pointi tatu zaidi ya Bayern Munich ambao mechi yao ya mwishoni mwa wiki iliahirishwa na iwapo wataishinda basi wataruka hadi kileleni. Dortmund wanasalia nafasi ya 5 wakiwa pointi kumi nyuma.

Vyanzo: Reuters/AFP